ASKOFU MWAMAKULA AMUWEKA WAKFU ASKOFU MPYA KENYA.
ASKOFU MPYA!
Kanisa la Moravian la
Uamsho Tanzania limemuweka wakfu Mch. Paul Kamau Kabaiya kuwa Askofu wa Kwanza
wa Kanisa la Moravian Kenya (The Moravian Church in Kenya) katika ibada
iliyofanyika katika Ushirika wa Ruiru, katika County ya Ruiru karibu na Nairobi
nchini Kenya jana tarehe 27/11/2017.
Ibada ya kumuweka
wakfu Askofu Kabaiya iliongozwa na Askofu Mkuu wa Dar es Salaam na Mkuu wa
Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania, Mhashamu Askofu Emmaus Bandekile
Mwamakula akisaidiwa na Maaskofu wawili wa Kanisa Anglikana la Kiinjili
Tanzania ambao ni Mheshimiwa Mhashamu Askofu Kuwayawaya Stephen Kuwayawaya
(Mvumi Makulu, Dodoma) na Mhashamu Askofu Edward Wilson (Kibondo, Kigoma) na
hivyo kufanya idadi ya Maaskofu waliomuweka wakfu kuwa watatu kama utaratibu na
kanuni ya Uaskofu wa mnyororo inavyotaka.
Mhashamu Askofu Paul
Kamau Kabaiya anakuwa pia ni Askofu Msaidizi wa Dar es Salaam na Askofu wa
Kenya.
Mhashamu Askofu Kabaiya alisoma Moravian
Theological College nchini Tanzania 1969 - 1971.
Alibarikiwa kuwa Mchungaji Shemasi mwaka 1972 na aliyekuwa Askofu wa Moravian Tanzania Jimbo la Magharibi (Tabora), Mhashamu Askofu Teofilo Kisanji (marehemu) na baadaye aliwekwa wakfu na Mhashamu Askofu Nikodemo wa Moravian Tabora kuwa Kasisi.
Baada ya kufanya kazi ya Uchungaji nchini Tanzania alirudi kwao Kenya kuanzisha Misheni ya Kenya ikiwa chini ya Jimbo la Tabora ambalo ndilo lilikuwa linalea Misheni ya Kenya.
Mwaka huu, Kanisa la Moravian Kenya limefanya maamuzi ya kuwa sehemu ya Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania hivyo kujiunga katika Fungamano la Makanisa ya Moravian ya Uamsho Duniani.
Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!
Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula - Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania.
Comments
Post a Comment