ASKOFU MWAMAKULA ATOA WITO KWA WATANZANIA NA AFRIKA JUU YA ZIMBABWE.
ZIMBABWE! ZIMBABWE! ZIMBABWE!
Kumekuwa na
sintofahamu nchini Zimbabwe tangu juzi.
Kikosi Kikuu cha Inkomo kiliripotiwa kuondoka
katika ngome yake na kuingia mjini na kuziba njia kuu.
Mkuu wa Majeshi alikaririwa akitoa onyo
akiambatana na Wakuu Waandamizi 90 wa Jeshi la Zimbabwe.
Umoja wa Vijana wa
ZANU PF ulipaza sauti kulitaka Jeshi la Nchi kutoingilia siasa. Hatimaye
imeripotiwa kuwa Jeshi limekitwaa Kituo cha Taifa cha Utangazaji huku taarifa
zikiarifu kuwa Ikulu imezingirwa.
Jeshi limearifu zaidi
kuwa halimlengi Rais Robert Mugabe bali linawalenga 'wahalifu' wanaomzunguka
Rais huyo na kuharibu au kuyumbisha uchumi na ustawi wa nchi.
Jeshi limearifu zaidi kuwa hali ya Rais na familia
yake iko salama.
Hatuhitaji kuingilia mzozo wa ndani wa
Zimbabwe wala sio kazi yetu kunyoosha kidole kuonyesha nani mkosaji na nani
yuko sahihi.
Nilopokuwa Uingereza mwanzoni na katikati ya miaka ya 2000 nilikutana na Wa-Zimbabwe wengi (Mashona na Mandebele) walioikimbia nchi yao kutokana na sintofahamu ya kisiasa iliyokuwa katika nchi yao.
Niliporejea nchini niliwakuta wengine hata huku. Wa-Zimbabwe ni ndugu zetu na ni binadamu wanaohitaji amani na utulivu katika nchi yao.
Watakaothirika zaidi katika vurugu zinazoendelea kule ni watoto, wanawake, wazee na wagonjwa.
Ninatoa wito kwa wanaombi wote na Watanzania wote na Afrika yote kuiombea Zimbabwe.
Tuombe pia kwa ajili ya Kanisa nchini Zimbabwe ili lisimame katika nafasi yake na kuwa nuru katika saa na wakati kama huu. Tuombe ili mzozo unaoendelea Zimbabwe miongoni
wanaoendesha nchi ile umaridhike haraka na kwa amani.
Tuombe hekima ya Mungu miongoni mwa nchi nyingine ambao ni washika dau katika uchumi na siasa za Zimbabwe.
Nchi yetu ni mdau mkubwa wa Zimbabwe. Tuombe hekima ya Mungu kwa ajili ya wanadiplomasia wetu wakiongozwa na Rais wetu Dkt. John Magufuri pamoja na Marais wetu wastaafu.
Mwanakondoo Ameshinda! Tumfuate!
Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula - Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania.

Comments
Post a Comment