MWITA ATOA NENO KWA WENYEVITI WANAOUZA MAENEO YALIYOPO MABONDENI.
NA CHRISTINA MWAGALA,OFISI YA MEYA WA JIJI
MSTAHIKI Meya wa jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita amewataka
wenyeviti wa serikali za mitaa kuepuka kujihusisha kwenye suala la uuzwaji wa
maeneo yaliyopo mabondeni, yasiyopimwa na yenye migogoro.
Aidha Mwita amewaomba waandishi wa habari kuongoza wananchi
katika suala la upandaji wa miti kwenye maeneo wanayoishi.
Mwita amesema kuwa wenyeviti ndio wasimamia wa maeneo hayo
na kwamba wanapaswa kujiepusha na mambo hayo kwani kufanya hivyo ni
kujiingiza kwenye migogoro isiyokuwa ya lazima na kuwasababishia wananchi
kupata usumbufu wa mafuriko nyakati za mvua.
Kauli ya Meya Mwita imekuja ikiwa ni baada ya kurejea
Jijini hapa akitokea Ujerumani alipokuwa kwenye mkutano wa
Mabadiliko ya Tabia ya nchini uliohusisha Mameya wote Duniani, na wataalamu wa
masuala ya mabadiliko hayo.
Meya Mwita amefafanua kuwa wenyeviti wa serikali za mitaa
ndio wanaosimamia makazi ya wananchi ikiwemo kushugulikia suala la upimaji na
kwamba wanalojukumu kubwa la kuhakikisha kuwa wanaepuka kushiriki katika suala
hilo la uuzwaji wa maeneo ambayo yana asili ya mikondo ya maji.
“ Nikweli kumekuwa na migogoro ya namna hii, sasa ni jukumu la kila kiongozi kwenye mtaa wake asikubali kujihusisha kwenye uuzwaji wa maeneo ambayo hayajapimwa, yaliyopo mabondeni, kufanya hivi nikujiletea matatizo kwao na kwa wananchi pia” amesema Meya Mwita.
Akizungumzia suala la upandaji miti, Meya Mwita amesema kuwa kila mwananchi anapaswa kupanda miti kwenye maeneo wanayoishi na akasisitiza kuwa waandishi wa habari wanatakiwa kuwa mfano kwenye maeneo yao.
“ Suala la upandaji miti ni jukumu la kila mmoja, lakini katika jiji langu, niwaombe waandishi wa habari muwe mfano kwenye hili ,kwakuwa nyie ndio kikoo cha jamii, iwe upanga, ama umejenga unapaswa kupanda mti kwenye eneo lako” amesisitiza Meya Mwita.
Mwita aliongeza kuwa” hata mimi Meya wenu nimepanda miti kwenye eneo lango, lakini pia nitaendelea kupanda, lakini mtakapounga mkono jambo hili wananchi pia watapata hamasa kubwa kutoka kwenu.


Comments
Post a Comment