TAARIFA KUTOKA JESHI LA POLISI MKOANI MBEYA.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu na ajali za barabarani.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaongeza jitihada za kuzuia na kupunguza ajali za barabarani kwa kuhakikisha madereva na watumiaji wengine wa barabara wanatii sheria za usalama barabarani. Aidha kumekuwa na ajali 01 ya kifo kama ifuatavyo:-
Mnamo tarehe 26.11.2017 majira ya saa 10:00 Asubuhi huko Maeneo ya Kadege, Kata ya Forest, Tarafa ya Iyunga, Jiji na Mkoa wa Mbeya, Gari yenye namba za usajili T.913 BEW aina ya Toyota Ipsum iliyokuwa ikiendeshwa na dereva aitwaye MUGANIZI RAPHAEL [34] Mkazi wa Simike iligongana na gari yenye namba za usajili T.204 CSZ/T.670 BEZ aina ya Scania Lory ikiendeshwa na HOSEA S/O MWASHAMBWA [28] Mkazi wa Uyole na kusababisha kifo kwa dereva wa Gari yenye namba za usajili T.913 BEW Toyota Ipsum.
Chanzo cha ajali ni mwendo kasi wa gari yenye namba za usajili T.913 BEW Toyota Ipsum hasa ukizingatia eneo hilo ni lenye mteremko mkali. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Rufaa Mbeya. Dereva wa lori alikimbia mara baada ya ajali na juhudi za kumtafuta zinaendelea. Upelelezi unaendelea.
Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na matukio makubwa ya uhalifu pamoja na wahalifu. Jitihada zinaendelea kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha Mkoa wetu unakuwa mahala salama. Hata hivyo Kumekuwa na matukio 02 ya mauaji kama ifuatavyo:-
Mnamo tarehe 25.11.2017 majira ya saa 22:06 usiku huko katika Kijiji cha Ipwizi, Kata ya Mjele, Tarafa ya Usongwe, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Mkoa wa Mbeya, Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la MINZA PAUL [25] Mkazi wa Ipwizi alifariki dunia baada ya kupigwa na fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na mume wake aliyefahamika kwa jina SHILONDI MAKWENGE ambaye alitoroka baada ya tukio.
Inadaiwa kuwa chanzo cha tukio hilo ni baada ya mume wa marehemu kurudi nyumbani akiwa amelewa kwa usafiri wa Pikipiki na kumwambia mke wake amlipe pesa dereva bodaboda aliyemlita nyumbani lakini mke wake alimjibu kuwa hana fedha na ndipo SHILONDI MAKWENGE alianza kumpiga mke wake na kusababisha kifo chake.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali Teule ya Ifisi kwa uchunguzi wa kitabibu. Jitihada za kumtafuta mtuhumiwa zinaendelea.
Mnamo tarehe 26.11.2017 majira ya saa 15:00 Alasiri huko Mtaa wa Itumbi uliopo Kata ya Matundasi, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, Mtu mmoja mkazi wa Itumbi aliyetambulika kwa jina la FLORIAN KAGOMBE [46] aliuawa baada ya kushambuliwa kwa kupigwa sehemu mbalimbali za mwili wake na kitu butu na walinzi wa kampuni ya “Itumbi Reaching Plant” ambao ni 1. IMANI KAYUNI [36] Mlinzi – Panic Security Group na 2. KELVIN NGONYANI [32] Mlinzi – Panic Security Group.
Inadaiwa kuwa, kabla ya kifo chake marehemu alikutwa na walinzi hao eneo la Kampuni ya “Itumbi Reaching Plant” inayojishughulisha na uchenjuaji dhahabu majira ya saa 02.00 usiku na kutiliwa shaka kuwa ni mhalifu/mwizi na hivyo kuanza kumpiga na kumwachia akiwa tabani.
Watuhumiwa wote wawili wamekamatwa na uplelelezi unaendelea. Aidha mwili wa marehemu umehifadhi Hospitali ya Wilaya ya Chunya kwa uchunguzi zaidi wa kitabibu.
TAARIFA YA UCHAGUZI MDOGO WA UDIWANI KATA YA IBIGHI, WILAYA YA RUNGWE.
Mnamo tarehe 26.11.2017 kumefanyika zoezi la uchaguzi wa marudio kwa nafasi ya udiwani. Kwa hapa Mkoa wa Mbeya, zoezi hili limefanyika katika Kata ya Ibighi Wilaya ya Rungwe ambapo nafasi hiyo ilikuwa ikigombaniwa na wagombea watano.
Kwa mujibu wa msimamizi wa uchaguzi kata ya ibighi ndugu STEVEN STANFORD MWAKINGWE ambaye pia ni Afisa Mtendaji Kata ya Ibighi alisema, Jumla ya watu waliotarajia kupiga kura katika kata hiyo ni 4,737 jumla ya vituo vya kupigia kura vilikuwa 13. Idadi halisi ya watu waliopiga kura ni 2,691, kura halali 2,672 na kura zilizoharibika ni 19.
Matokeo rasmi ya uchaguzi huo ni kama ifuatavyo:-
CCM: SUMA IKENDA FYANDOMO – Kura 1,205
CHADEMA: SIMBA LUSUBILO EMANUEL – Kura 1,449
CUF: GRACE NGALABA – Kura 12
UDP: GEOFREY MWAKAJINGA – Kura 02
DP: EMANUEL ANDONGOLILE MWAFILAMBO – Kura 0.
Kutokana na matukio hayo, Msimamizi wa Uchaguzi ndugu STEVEN STANFORD MWAKINGWE alimtangaza rasmi SIMBA LUSUBILO EMANUEL kuwa mshindi na Diwani wa Kata ya Ibighi.
Katika zoezi hilo, hali ya ulinzi na usalama iliimarishwa na zoezi la uchaguzi lilifanyika kwa hali ya amani na utulivu.
WITO:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishina wa Polisi MOHAMMED R. MPINGA anatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa za mahali alipo mtuhumiwa wa tukio la ajali azitoe ili akamatwe na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.
Pia Kamanda MPINGA anatoa wito kwa madereva kuwa makini ikiwa ni pamoja na kufuata sheria na alama za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoepukika. Aidha Kamanda MPINGA anaendelea kutoa wito kwa wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za mtu/watu wanaowatilia mashaka katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na wahamiaji haramu kwa hatua zaidi za kisheria.
[MOHAMMED R. MPINGA – DCP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA
Comments
Post a Comment