WANANCHI WAELEZEA JINSI GLOBAR MINING ALIVYOWAVUNJIA NYUMBA ZAIDI YA 50.

 Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Salasala Kata ya Wazo, Hashimu Semboja  kulia aliyeyevaa tisheti nyeupe, kulia ni Jakson Kakiziba akibishana na Mwenyekiti juu ya wananchi kwenda kusafisha  eneo hilo.

  Jakson Kakiziba kushoto katikati ni Mwandishi wa Habari wa Chanel Ten Fred Mwanjala na kulia ni mtoto wa Mkurugenzi wa Kampuni ya  Global Mining  Jerry Kakiziba ambao walifika eneo hilo baada ya wananchi kuanza kusafisha.

 Baadhi ya wananchi ambao walibomolewa nyuza hizo mwaka 2010 na  Kampuni ya Global Mining inayomilikiwa na Jerry Kakiziba, wakisafisha eneo hilo.


 Wananchi waliobomolewa nyumba zao wakiendelea kufyeka eneo hilo, lengo ni kurudi kwenye eneo hilo.

  Mtoto wa Mkurugenzi wa Kampuni ya Global Mining inayomilikiwa na Jerry Kakiziba  akiwa amesimama akishuhudia kinachoendelea kwenye eneo hilo, pembeni yake ni lori linalochukua kokoto kwenye eneo ambalo Serikali ilishafunga machimbo hayo tangu 2006. 

 Baadhi ya wananchi waliofika eneo hilo jana.


 Wananchi wakiwa wamesimama wakishuhudua kinachoendelea hapo, huku wakiendelea kutoa malalamiko juu ya Kampuni ya Global Mining kwa kitendo ambacho amekuwa wakiwafanyia wananchi hao.
 Baadhi ya wananchi wakishuhudia kinachoendelea, nyuma yao ni moja ya nyumba ambayo Mkurugenzi wa Kampuni hiyo alijimilikisha baada ya kubomoa nyumba zote.

 Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Salasala Kata ya Wazo, Hashimu Semboja , aliyevaa tisheti jeupe akiwa na  baadhi ya wananchi waliofika eneo hilo.

Wananchi wakiondoka kwenye eneo hilo jana.


Na Mwandishi Wetu.

WAKAZI wa Salasala Mtaa wa Luona  wameelezea jinsi Kampuni ya Globar Mining inayomilikiwa na Jerry Kakiziba ilivyowanyanyasa na kuwavunjia nyumba zaidi ya 50 na kuwanyanganya eneo lao.

Aidha, wameiomba Serikali  kupitia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kuwasaidia kutatua  mgogoro huo wa ardhi  kama alivyosaidia maeneo mengine .

Wakizungumza na waandishi wa habari jana wakazi hao ambao walienda kufyeka eneo hilo kwa lengo la kurudi  kwenye eneo lao walisema hawana sehemu ya kuishi  na hivyo wanalazimika kurudi katika eneo ambao lilikuwa ni makazi yao.

Naye, Matheo Haule  alisema  wao walikuwa wachimbaji wadogo kwenye eneo hilo ila baada ya Serikali kufunga machimbo hayo  2006 waligawana viwanja hivyo na kujenga nyumba zao.

Alisema baada ya kujenga nyumba zao Kampuni ya Glober Mining ambaye naye alikuwa miongoni mwa Makampuni makubwa yaliyokuwa yakichimba machimbo maeneo hayo  ilienda na kuvamia eneo hilo mwaka 2010 na kuvunja nyumba zao.

“Baada ya Serikali kufunga machimbo haya ya kokoto mwaka 2006 sisi tuligawana viwanja eneo ambalo tulikuwa  tunachimba na kujenga nyumba, lakini mwaka 2010 Kampuni ya Glober Mining ilikuja na kuvamia eneo letu na kutuvunjia nyumba zaidi ya 50,”alisema Haule na kuongeza

 “Mmiliki huyu   licha ya kutubomolea nyumba ameendelea kutoa vitisho kwetu na kutunyanyasa  kwa kutumia nguvu za dola kila tunapotaka kurudi kwenye eneo,”

Alisema pamoja na kuvunja nyumba zote hizo na kubakisha nyumba moja ambayo “Ilikuwa nyumba yangu na anaendelea kuitumia kwa kuwahifadhi ndugu zake ambao wamekuwa wakilinda eneo hili,”

Abdara Njole, alisema wanaiomba Serikali iingilie kati kwani Nchi hii  bado ina mabepari wakubwa na wanao nyanyasa  wananchi walio  katika hali ya chini kwa kutumia fedha zao.

“Huyu bwana ni mtu maarufu Serikalini na ni mtu mwenye fedha nyingi sana na anauwezo wa kukukamata na kukubambikia kesi na huwa anatwambia tutakapo rudi hapa sisi tutakuwa halali yake kwa chochote kitakachotokea,”

Paulo Pasco alisema   Mkurugenzi huyo  amekuwa akiwaambia kuwa Serikali ameiweka mikononi na hakuna ofisi ambayo itawasikiliza wao kwani ofisi zote zimejaa Wahaya na Wahaya wote ni ndugu zake.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Salasala Kata ya Wazo, Hashimu Semboja alisema mgogoro huo aliukuta baada ya kuingia madarakani 2015 .
Alisema wananchi hao walipeleka malalamiko kwenye ofisi yake na kumueleza jinsi Kampuni hiyo ilivyowabomolea nyumba zao na baada ya malalamiko hayo aliamua kujiridhisha.

 Alisema hakuishia hapo aliendelea kufuatilia suala hilo kwenye ngazi za juu ili kujiridhisha zaidi Mmiliki halali wa eneo hilo ila alibaini kuwa Globar Mining sio Mmiliki wa eneo hilo ila alikuwa na kibali cha kuchimba na sio kumiliki ardhi.

“Mimi nashangazwa sana uhalali wa Globar Mining uko wapi, huyu mtu ni mbabaishaji akiambiwa alete vielelezo vya umiliki wa eneo hili anasema anaendelea kushughurikia vielelezo,”alisema Semboja

“Hii sehemu sio yake  ilikuwa  ya  wachimbaji wadogo lakini baada ya Serikali kufunga machimbo haya  mwaka 2006 makampuni makubwa yaliondoka, ila Kampuni ya Globar Mining ilibaki na kuendelea kuchimba,”alisema

“ Eneo lake ni   lile kule nyumba ambalo alikuwa akilitumia kabla machimbo hayajafungwa  ila  alivamia  eneo walilokuwa wakitumia  wachimbaji wadogo   na kuwavunjia nyumba zao,”

“ Baada ya kufuatilia na kujua ukweli juu ya eneo hili  nilimuandikia barua aje  Ofisi ya Serikali ya Mtaa kujieleza juu ya unyanyasaji anaoendelea kuufanya kwa wanachi ambao aliwabomolea nyumba zao ila cha kushangaza alitujibu kwa kutuma onyo juu ya kufuatilia suala hili,”

Alisema eneo hilo lingeweza kutumika kwaajili ya kujenga huduma za jamii ikiwamo Soko, Ofisi ya Serikali ya Mtaa, Shule na Hospitali kwani mtaa wake  hauna huduma za kijamii na pia lingetolewa kwaajili ya wale wananchi 51ambao walivunjiwa nyumba zao na Globar Mining.

Pia Mwenyekiti alilalamikia kitendo cha Kampuni hiyo kuendelea kuchimba mawe kinyume na sheria kwenye  eneo hilo ambalo Serikali ilishafunga tangu mwaka 2006 na uchimbaji huo umekuwa ukiwaletea athari  watoto wadogo na wengine wamekuwa wakipoteza maisha.

Hata hivyo mmoja wa wadogo wa Mkurugenzi wa Kampuni hiyo ambaye alijitambulisha kwa jina la Jakson Kakiziba alisema eneo hilo wanalimiliki kihalali na wana nyaraka zote  za umiliki wa eneo hilo.


Comments

Popular posts from this blog

ASKOFU MWAMAKULA AMUWEKA WAKFU ASKOFU MPYA KENYA.

NABII ELIYA AZIDI KUFUNGUA WATU WALIOFUNGWA WENYE VIFUNGO MBALIMBALI.

RAIS WA ZANZIBAR DK SHEIN AZUNGUMZA NA MFALME WA DUBAI, WAFANYABIASHARA, ATEMBELEA BANDARI WA JEBEL ALI PORT NA KUTEMBELEA MRADI WA AKHEEL