MBINU SAHII  ZA  KUIMARISHA AFYA YA KINYWA  NA MENO.


 Daktari bingwa wa meno kutoka Chuo kikuu cha AJMANI cha Falme za kiaarabu,  Zaid Mohammed Hassan akimfanyia uchunguzi wa meno mwanafunzi wa skuli ya Mwanakwerekwe H Juma Hassan katika zoezi la kutoa matibabu yaliofanyika skulini hapo.



Na Kijakazi Abdalla-MAELEZO
JAMII imetakiwa itumie mbinu sahihi ili kuimarisha afya kinywa na meno na kupunguza mzigo mkubwa wa kutibu maradhi ya meno.  

Akizungumza katika kampeni maalum juu ya kujikinga na maradhi yanayoathiri kinywa na meno katika skuli ya msingi Mwanakwerekwe ‘E’, Daktari Dhamana Kanda ya Unguja Muhidin Abdalla Mohammed, amesema wananchi wengi wamebainika kuathiriwa na maradhi ya kinywa na meno.

Kwa hivyo amesema ipo haja ya kuchukua tahadhari ili kupunguza tatizo hilo. Aidha, alisema lengo la kampeni hiyo ni kuinua uwelewa wa watu ambao hawatoi kipaumbele kwa afya ya kinywa na meno, na hivyo kujikuta wakisumbuka kuhahangaikia matibabu.

 Dkt. Muhidini Abdalla wa meno kanda ya Unguja  akiwapatia elimu fupi wanafunzi wa skuli ya Mwanakwerekwe E namna ya kusafisha meno.

Dk. Muhiddin pia amesema hatua ya kufanya kampeni hiyo katika skuli, inalenga kuwapa elimu wanafunzi juu ya namna bora na sahihi za kutunza meno na kupiga mswaki ili waimarishe afya ya meno yao.

Alisema katika umri mdogo, ndipo watoto hupitia mabadiliko makubwa kimwili, hivyo kuwapa taaluma kutawawezesha kufahamu mbinu sahihi za kuimarisha afya na kujikinga wanapokua wakubwa.

Hata hivyo, ameiomba Serikali iongeze juhudi zaidi kufikisha huduma za meno kila eneo ingawa kunahitaji gharama kubwa, lakini akasema kuacha watu waugue bila tiba ni gharama zaidi.

Alieleza kuwa, tangu kuanza kampeni hizo kuelekea maadhimisho ya siku ya afya ya kinywa na meno kimataifa, zaidi ya watoto 1,000 wametibiwa kwa kushirikiana na madaktari kutoka Ujerumani, Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE) pamoja na Wizara ya Afya.

 Daktari dhamana wa Meno kanda ya Unguja alievalia vazi jeupe Muhidini Abdalla akishirikiana na madaktari bingwa kutoka Ujerumani na Falme za Kiarabu wakimng’oa jino mwanafunzi Aisha Makame wa skuli ya Mwanakwerekwe H katika matibabu yaliofanyika skulini hapo.

Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Msingi Mwanakwerekwe ‘E’ Khitiyar Haidhuru Ramadhani,  alisema ujio wa madaktari hao umewapa faraja  wanafunzi na elimu sahihi ya kutunza meno yao.

Aidha aliwataka wazee kujenga utamaduni wa kuwanunulia watoto vitu vinavyoweza kuwaepusha na maradhi ya meno kama vile pipi, biskuti na chokoleti ambavyo huchangia zaidi maradhi hayo.

Mwalimu huyo pia aliwaomba wazazi kuwasimamia vyema watoto na kuhakikisha wanapiga miswaki mara mbili kwa siku na kwa njia sahihi kwani imebainika kuna baadhi ya wanafunzi huenda skuli bila kusafisha meno yao.

Aidha aliiomba Wizara ya Afya iliendeleze zoezi la  kuchunguza maradhi yote kwa wanafunzi, kwani kumekuwa na ongezeko kubwa la maradhi lakini  baadhi ya wazee hawamudu gharama za uchunguzi na tiba.
 Mwanafunzi  Ali Makame wa skuli ya Mwanakwereke E akiwaonesha mfano wa kusafisha meno wanafunzi wezake baada ya kupatiwa elimu ya usafishaji wa meno skulini hapo.
  Daktari bingwa kutoka Ujerumani, Isabella Di Lorenzo akimfanyia uchunguzi wa meno mwanafunzi wa skuli ya Mwanakwerekwe H Raiyani Subeti Mkaazi wa Magomeni katika matibabu yaliofanyika skulini hapo.
Mwalimu Mkuu wa skuli ya Mwanakwerekwe E, Khityar Haidhuru Ramadhan  akizungumza na waadishi wa habari kuhusuana na zoezi hilo na kuishukuru Wizara ya Afya Zanzibar kwa kuwapatia matibabu wanafunzi wa skuli hizo. (Picha na Abdalla Omar Habari Maelezo).

Comments

Popular posts from this blog

ASKOFU MWAMAKULA AMUWEKA WAKFU ASKOFU MPYA KENYA.

NABII ELIYA AZIDI KUFUNGUA WATU WALIOFUNGWA WENYE VIFUNGO MBALIMBALI.

BONANZA LA BAJAJ, BODABODA LAFANA DAR