ASKOFU MWAMAKULA “ UNYANG'ANYI HUU KUOTA MIZIZI KATIKA NCHI YETU”!
Siku moja nilikwenda katika Ofisi ya Mkuu wa
Wilaya mojawapo jijini Dar es Salaam.
Moja ya mambo
niliyoyakuta kule ni malalamiko ya mwanamke mmoja ambaye nyumba yake ilikuwa
inaelekea kupigwa mnada.
Yule mwanamke alikuwa amekopa katika Taasisi
mojawapo ya kukopesha, kiasi alichokuwa amekopa hakikuzidi shilingi milioni
tatu.
Alijitahidi kulipa lakini alishindwa kumalizia
kiasi cha shilingi takribani laki tisa lakini Taasisi ile iliamua kuipiga mnada
nyumba ya yule mama.
Katika kuulizwa, ilidhihirika wazi kuwa yule
mama alikuwa hajui matokeo na madhara ya kuchelewa kurudisha mkopo wake kwa
wakati.
Vipengere vilivyowekwa katika mkataba ule
viliwaruhusu wakopeshaji kufilisi mali za mkopaji ikiwemo kupiga mnada nyumba
yake.
Pia, taasisi nyingi za kukopesha zimeweka vipengere
ambavyo vinazipa Taasisi hizo kupiga mnada mali za wateja wao zikiwemo nyumba
hata kama kiasi kinachodaiwa hakiendani na thamani ya nyumba.
Tumefuatilia na
tumejiridhisha kwa kiasi kikubwa kuwa watu wengi wameathirika na wengine
wanaendelea kuathirika kutokana na Taasisi za mikopo kupiga mnada nyumba hata
zenye thamani kubwa kwa deni hata la shilingi laki tano!
Ili kuzuia hali hii tunaomba wateja walindwe
kama wakopeshaji wanavyolindwa na vipengere vya makubaliano.
Tunaomba Mamlaka zinazohusika ziwabane wakopeshaji wote kuweka wazi masharti yao kwa wateja wao kabla ya kuwapa mikopo.
Tunashauri utaratibu uwepo kuhakikisha kuwa mkopaji asikope pasipo kupata ufafanuzi wa masharti ya mkopo wake kutoka kwa mwanasheria ambaye atasaini sehemu ya mkataba na kwamba awe ni mwanasheria huru ambaye gharama zake zitapangwa na mamlaka husika.
Tunashauri kuwa mkopo wowote ambao utahusisha kufilisi nyumba, kiwanja, shamba, kiwanda, gari, nk ni lazima mkopaji awe amepata ushauri na ufafanuzi wa vipengere vya mkataba kutoka kwa wataalam wa mikopo na wanasheria wasiohusika na mkopeshaji!
Vingenevyo, kuna hatari wajanja wakaendelea kujinufaisha kwa kupora mali za wanyonge! Tukiruhusu hali hii kuendelea itakuwa ni sawa na kuruhusu unyang'anyi uliohalalishwa kisheria.
Na huu ndio ujumbe wangu wa PASAKA kwa waumini na Watanzania wote.
Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!
Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula - Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania na Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Makanisa ya Moravian ya Uamsho Duniani.

Comments
Post a Comment