MKUU WA MKOA GEITA AWATAKA WANANCHI KUJITOKEZA KWA WINGI KWENYE KAMPENI YA ELIMU KWA MLIPAKODI.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe.
Mhandisi Robert Luhumbi, akizungumza na waandishi wa habari juzi mkoani
humo kuhusu Kampeni Maalum ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi iliyoanza juzi hadi 13 Aprili, 2018 ikiwa na lengo la
kuelimisha, kusikiliza malalamiko, changamoto pamoja na kupokea maoni
mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara na wananchi wa mkoa huo.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
Mkoa wa Geita akizungumza wakati wa mkutano wa waandishi wa habari mkoani humo
kuhusu Kampeni Maalum ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi iliyoanza juzi hadi 13
Aprili, 2018 ikiwa na lengo la kuelimisha, kusikiliza malalamiko, changamoto
pamoja na kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara na wananchi wa
mkoa huo.
Kiongozi
wa timu ya watalaam kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu
Maternus Mallya akizungumza wakati wa mkutano wa waandishi wa habari mkoani
Geita kuhusu Kampeni Maalum ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi iliyoanza juzi
hadi 13 Aprili, 2018 ikiwa na lengo la kuelimisha, kusikiliza malalamiko,
changamoto pamoja na kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara na
wananchi wa mkoa huo.
Na Veronica Kazimoto
Geita
Wito umetolewa kwa wafanyabiashara na wananchi
wa Mkoa wa Geita kujitokeza kwa wingi katika Kampeni Maalum ya Huduma na Elimu
kwa Mlipakodi kwa ajili ya kuwasilisha malalamiko, changamoto, maoni
pamoja na kupata elimu ya masuala ya kodi na ukusanyaji wa mapato ya Serikali
kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa habari leo mkoani
Geita, Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Mhandisi Robert Luhumbi amesema kuwa,
wafanyabishara na wananchi watumie fursa ya kampeni hii itakayomalizika tarehe
13 Aprili, 2018 kupata elimu sahihi ya masuala ya kodi na tozo mbalimbali.
"Nachukua fursa hii kutoa wito kwa
wafanyabiashara na wananchi wote wa mkoa huu hususani wale wanaoishi katika
maeneo ya Masumbwe, Ushirombo, Rulembela, Katoro, Lunzewe, Namonge,
Nyanghw'ale, Bwanga na Muganza kujitokeza kwa wingi ili waweze
kujifunza, kupata huduma na kutoa maoni yao kwa watalaam wetu wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) ili waweze kuyatolea ufafanuzi na kuyafanyia kazi,"
amesema Mhe. Luhumbi.
Nae Meneja wa TRA mkoani hapa, James Jilala
amesema kuwa, lengo kuu la kufanya kampeni hii maalumu ni kuelimisha,
kusikiliza malalamiko, changamoto pamoja na kupokea mrejesho na maoni
mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.
"Kampeni hii ni mwendelezo wa Wiki ya
Elimu kwa Mlipakodi iliyofanyika nchi nzima kuanzia tarehe 5 hadi 9 Machi, 2018
katika ngazi ya mkoa. Kutokana na matokeo ya kampeni ile mkoani hapa, tumeona
ni muhimu tuwe na kampeni nyingine maalumu ambayo inafanyika maeneo mbalimbali
katika wilaya zetu tofauti na ile ya kwanza iliyofanyika Geita mjini tu,"
amefafanua Jilala.
Kwa upande wake kiongozi wa timu ya watalaam
kutoka TRA Makao Makuu Maternus Mallya ameeleza kuwa, timu yake imejipanga
vizuri na tayari kazi imeanza kufanyika katika vituo vyote vilivyotengwa kwa
ajili ya kampeni hiyo.
"Hapa ninapozungumza, wenzangu wako
kwenye maeneo husika wanaendelea kufanya kazi. Hivyo, kama alivyosema Mhe. Mkuu
wa Mkoa, nami natoa rai kwa wananchi wote mkoani hapa, kujitokeza kwa wingi ili
waweze kukutana na watalaam wetu kwa ajili ya kupata huduma na elimu ya
mlipakodi," amesema Mallya.
Kampeni Maalum ya Huduma na Elimu kwa
Mlipakodi mkoani Geita imeanza leo tarehe 9 hadi 13 Aprili, 2018 ambapo pamoja
na mambo mengine, wafanyabiashara na wananchi watasajiliwa na kupatiwa Namba ya
Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) pamoja na kuelimishwa kuhusu ulipaji wa Kodi ya
Majengo kwa njia ya kieletroniki.



Comments
Post a Comment