SERIKALI YASISITIZA HAKUNA UPOTEVU WA SHILINGI TRILIONI 1.5
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akitoa maelezo kuhusu mikakati ya Serikali kuhakikisha kuwa kila kipande cha ardhi hapa nchini kinapimwa ili kuchochea maendeleo wakati wa kipindi cha maswali na majibu leo Bungeni mjini Dodoma.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji akitoa taarifa ya Serikali kuhusu hoja ya kutoonekana kwenye matumizi ya Serikali shilingi trilioni 1.51 leo Bungeni mjini Dodoma.
Mbunge wa viti maalum (CCM) Mkoa wa Kagera Mhe. Oliver Semuguruka akichangia hoja ya Bajeti ya Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto kuhusu maboresho yanayopaswa kufanywa katika sekta ya afya ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi katika Mkoa wa Kagera na katika hosipitali zote za umma.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni akisisitiza kuhusu mikakati ya Jeshi la Polisi kuendelea kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao kote nchini leo Bungeni mjini Dodoma wakati wa kipindi cha maswali na majibu.
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson akijibu miongozo ya wabunge mapema leo Bungeni mjini Dodoma mara baada ya kipindi cha maswali na majibu.
Sehemu ya wageni waliofika Bungeni kwa ziara ya mafunzo wakifutilia kipindi cha maswali na majibu leo Bungeni mjini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Kazi Vijana Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (kulia) akifurahia jambo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.(Picha zote na Frank Mvungi- MAELEZO
Serikali leo imelithibitishia Bunge na umma kwa ujumla kuwa kufuatia maneno ya baadhi ya watu yaliyosheheni upotofu, siasa na yenye nia ya kuchafua taswira ya nchi kwamba kuna Shilingi trilioni 1.5 zimepotea, ukweli ni kwamba hakuna upotevu huo na mchanganuo wa matumizi uko wazi.
Akitoa taarifa hiyo ya kina Bungeni leo, huku akiainisha mchanganuo wa matumizi ya fedha hizo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, amesisitiza kuwa chini ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli, fedha za umma ziko salama na wanaojaribu kufanya ufujaji hatua kali zinachukuliwa. Taarifa kamili yenye aya 12 ni kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 49 ya Kanuni za Bunge Toleo la Januari 2016, naomba kuwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu Kauli ya Serikali juu ya madai ya kutoonekana kwa matumizi ya shilingi trilioni 1.51 kwenye matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2012/13 hadi 2016/17, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango ilikuwa kwenye kipindi cha mpito cha miaka mitano ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa kuandaa hesabu za Serikali kwa kutumia mfumo wa Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu katika Sekta ya Umma (International Public-Sector Accounting Standards – IPSAS Accrual).
Katika kipindi hicho, Serikali iliendelea kukusanya taarifa mbalimbali kwa kutumia mfumo huu ili kutuwezesha kutambua kikamilifu hesabu za mali, madeni pamoja na mapato yanayotokana na kodi.
“IPSAS Accrual” ni mfumo wa kiuhasibu ambapo mapato yanatambuliwa baada ya muamala husika kukamilika na sio wakati fedha taslimu inapopokelewa; na matumizi yanatambuliwa wakati muamala wa matumizi umekamilika na sio wakati fedha inalipwa. Mfumo huu ni mzuri na una faida nyingi ikiwa ni pamoja na miamala ya Mapato na Matumizi kutambuliwa wakati husika na siyo wakati wa fedha taslimu inapopokelewa au kulipwa.
Mheshimiwa Spika, matokeo ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa uandaaji wa hesabu kwa mfumo wa “IPSAS Accrual” umeiwezesha Serikali na taasisi zake kutoa taarifa za kina na zinazoonesha uwazi na uwajibikaji wa taasisi husika, hususan katika usimamizi wa mali na madeni ya taasisi. Kuongezeka kwa uwazi, kumewawezesha watumiaji wa hesabu kupata taarifa zinazowasaidia kufanya maamuzi sahihi na kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, kutokana na matumizi ya mfumo huu wa viwango vya Kimataifa vya Uhasibu katika sekta ya umma, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu na Watanzania kwa ujumla kwamba hakuna fedha taslimu ya shilingi trilioni 1.51 iliyopotea au kutumika kwenye matumizi ambayo hayakuidhinishwa na Bunge. Hivyo basi, madai ya baadhi ya watu wasiolitakia mema Taifa letu na Serikali yetu ya Awamu ya Tano hayana msingi wowote wenye mantiki. Haya yanadhihirishwa na aya zifuatazo kwenye tamko hili la Serikali.
Mheshimiwa Spika, taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imeeleza jumla ya mapato yote ya Serikali kwa mwaka 2016/17, yalikuwa shilingi trilioni 25.3 ambapo fedha hizi zinajumuisha mapato ya kodi, mapato yasiyo ya kodi, mikopo ya ndani na nje pamoja na misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.
Mheshimiwa Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba, kuanzia mwaka 2016/17, Mamlaka ya Mapato Tanzania ilianza rasmi kuyatambua mapato kwa mfumo wa Accrual. Hivyo basi, kati ya mapato haya ya shilingi trilioni 25.3, yalikuwemo pia mapato tarajiwa (receivables) kama mapato ya kodi yenye jumla ya shilingi bilioni 687.3 pamoja na mapato ya kodi yaliyokusanywa kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya jumla ya shilingi bilioni 203.92 (transfer to Zanzibar).
Mheshimiwa Spika, katika uandishi wa taarifa ya ukaguzi, CAG alitumia taarifa za hesabu na nyaraka mbalimbali ikiwa ni pamoja na Taarifa za Utekelezaji wa Bajeti (Budget Execution Report) ambapo hadi kufikia tarehe 30 Juni 2017, mapato yalikuwa jumla ya shilingi trilioni 25.3 na matumizi yalikuwa shilingi trilioni 23.79. Matumizi haya hayakujumuisha shilingi bilioni 697.85 zilizotumika kulipa dhamana na hati fungani za Serikali zilizoiva. Matumizi haya yalikuwa hayajafanyiwa uhamisho (re-allocation) wakati ukaguzi unakamilika. Hivyo basi, baada ya kufanya uhamisho jumla ya matumizi yote kwa kutumia Ridhaa za Matumizi (Exchequer issues) yalikuwa shilingi trilioni 24.4.
Mheshimiwa Spika, kutokana na ufafanuzi huo, shilingi trilioni 1.51 zilizodaiwa kutoonekana kwenye matumizi ya Serikali zilitokana na mchanganuo ufuatao:
Maelezo Shilingi Trilioni
Matumizi ya dhamana na hati fungani zilizoiva 0.6979
Mapato tarajiwa (Receivables) 0.6873
Mapato ya kodi yaliyokusanywa kwa niaba ya Serikali ya Zanzibar 0.2039
Jumla 1.5891
Fedha iliyotolewa zaidi ya mapato (Bank Overdraft) (0.0791)
Fedha zilizodaiwa kutoonekana kwenye matumizi 1.51
Mheshimiwa Spika, hii inamaanisha kwamba, baada ya kupunguza mapato ya Zanzibar ya shilingi bilioni 203.92 na kupunguza mapato tarajiwa ya shilingi bilioni 687.3, mapato halisi kwa mwaka 2016/17 yalikuwa shilingi trilioni 24.41. Aidha, baada ya kujumlisha matumizi ya dhamana na hati fungani zilizoiva za kiasi cha shilingi bilioni 697.85 kwenye matumizi ya shilingi trilioni 23.79 yaliyooneshwa katika Taarifa ya CAG, ridhaa za matumizi zilizotolewa zilikuwa shilingi trilioni 24.49 na kuleta ziada ya matumizi ya shilingi bilioni 79.07 ikilinganishwa na mapato.
Kwa mchanganuo huu, ni dhahiri kwamba kwa mwaka 2016/2017 matumizi ya Serikali yalikuwa makubwa kuliko mapato kwa shilingi bilioni 79.09 ambazo ni Overdraft kutoka Benki Kuu ya Tanzania. Utaratibu wa kutoa fedha zaidi ya mapato (Overdraft facility) uko kwa mujibu wa kifungu cha 34 cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006.
Hitimisho
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imepata mafanikio makubwa katika uandaaji wa Hesabu za Serikali kwa kutumia mfumo huo wa Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu katika Sekta ya Umma (IPSAS Accrual). Itakumbukwa kwamba, katika Afrika, Tanzania ndio nchi pekee iliyofanikiwa kwa kiwango kikubwa kuandaa hesabu kwa kuzingatia matakwa ya IPSAS na kufanikisha kuandaa hesabu za Majumuisho kwa kuzingatia mfumo huo.
Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo haya ya Serikali, napenda kulitaarifa Bunge lako Tukufu na wananchi kwa ujumla kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ipo makini na haiwezi kuruhusu upotevu wa aina yoyote wa fedha za umma. Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuona kwamba, kila mapato yanayokusanywa yanatumika ipasavyo na kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii, na naomba kuwasilisha.
Comments
Post a Comment